KWALE UNITED YATINGA NUSU FAINALI YA RASHID ABDALLAH SUPER CUP KWA MARA YA KWANZA

Kwale United imeandika historia katika mashindano ya Rashid Abdallah Super Cup msimu wa saba baada ya kufuzu kwa hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.
Timu hiyo inayotoka katika mji wa Kwale ilijihakikishia nafasi hiyo baada ya kuwashinda majirani zao, Generation FC ya Msambweni, kwa mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia sare ya mabao 2-2 katika muda wa kawaida.
Ushindi huo umeiweka Kwale United katika hatua ya nne bora ya mashindano hayo, ikiendeleza matumaini ya kutwaa taji la msimu huu.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha mkuu wa Kwale United, Shaban Suleiman Alimaruf Follan, alisema kuwa licha ya timu yake kuanza vibaya na kuruhusu mabao mawili mapema, wachezaji wake walionyesha moyo wa kupambana na nidhamu ya hali ya juu kurejea mchezoni.
Alisema uwezo wa wachezaji wake kurejesha matokeo na hatimaye kushinda kwa mikwaju ya penalti unaonyesha ari na maandalizi waliyonayo kuelekea hatua zinazofuata.
Kocha huyo aliongeza kuwa kikosi chake kimejipanga kikamilifu kwa michezo ya nusu fainali, akisisitiza kuwa hakitachukulia hatua hiyo kama mchezo wa kawaida bali kama fursa nyingine ya kuweka historia katika mashindano hayo.
Aidha, aliwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na wadau wote wanaoiunga mkono timu hiyo, akisema mafanikio hayo yametokana na mshikamano na juhudi za pamoja.
Alisisitiza kuwa licha ya kufurahia hatua waliyofikia, lengo kuu la Kwale United msimu huu ni kufuzu kwa fainali na kupigania ubingwa.
