TULIFIKA LINI HAPA KAMA TAIFA? MIRADI YA MAENDELEO YAGEUKA UWANJA WA MIVUTANO YA KISIASA

Mzozo kati ya Rais William Ruto na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, kuhusu Soko la Kisasa la Masinde Muliro mjini Kitale ni jambo la kusikitisha
Katika siku za hivi karibuni, soko hilo limekuwa kitovu cha mvutano wa kisiasa baada ya Rais Ruto kulizindua Oktoba 16, 2026, huku Gavana Natembeya akipinga namna mradi huo ulivyochukuliwa na serikali ya kitaifa. Natembeya alisisitiza kuwa serikali ya kaunti ndiyo iliyojenga soko hilo kwa kutumia fedha za kaunti, huku Rais Ruto akisema serikali ya kitaifa ilichangia kukamilisha mradi huo.
Ikiwa ni kweli kwamba soko hilo lilijengwa na serikali ya kaunti kama anavyodai Natembeya, kwa nini Rais Ruto aingize mradi huo katika mvutano wa kisiasa badala ya kutambua mchango wa kaunti na kuhakikisha wananchi wananufaika?
Ni muhimu kuelewa kwamba suala la nani alifadhili ujenzi, nani alichangia kukamilisha mradi na nani anapaswa kusimamia soko ni mambo yanayopaswa kuthibitishwa kwa nyaraka na sheria. Hakuna kiongozi anayepaswa kupewa sifa zisizostahili, lakini pia hakuna anayepaswa kunyimwa utambuzi wa mchango wake.
Swali tu nauliza hapa Kwa nini tunafika mahali ambapo viongozi wanashindana kuhusu majina yao kuwekwa kwenye miradi, ilhali wananchi wanaohitaji huduma ndio wanaopaswa kuwa kipaumbele?
Rais Ruto bila shaka anaelewa kuwa wananchi hawaangalii tu nani amefungua soko, amekata utepe au nani ameweka jina lake kwenye bango. Wananchi wanaangalia maendeleo ambayo yamefanyika katika maisha yao. Wanataka kujua ni nani amewajengea barabara, nani ameboresha hospitali, nani amewapa wafanyabiashara mazingira bora ya kufanya kazi na nani ametimiza ahadi alizotoa wakati wa kutafuta kura.
Vivyo hivyo, Gavana Natembeya anapaswa kuhakikisha kuwa madai yake kuhusu ufadhili wa soko yanaungwa mkono na rekodi zilizo wazi, na kwamba wafanyabiashara waliokuwa wameathiriwa na ujenzi wanapata nafasi za kufanya biashara kwa utaratibu na haki.
Ikiwa mradi huo ni wa serikali ya kaunti, mchango wa kaunti utambuliwe. Ikiwa serikali ya kitaifa ilichangia kukamilisha mradi huo, mchango wake pia utambuliwe. Lakini hakuna upande unaopaswa kuutumia mradi huo kama silaha ya kisiasa.
Jambo la msingi ni kwamba mradi huo unapaswa kuwahudumia wananchi wa Kitale na Trans Nzoia kwa ujumla.
Soko likiwa tayari kutumika, wafanyabiashara wapatiwe nafasi kwa utaratibu wa haki na uwazi. Wasibaguliwe kwa misingi ya kisiasa, wala wasiachwe nje kwa sababu tu hawana uhusiano na viongozi fulani. Mwisho wa siku Lengo la soko ni kuwawezesha wananchi kujipatia riziki, si kuwapa viongozi nafasi ya kujitangaza kisiasa.
Hata hivyo, jambo hili lisigeuke kuwa mazoea katika taifa letu. Kila kiongozi anapaswa kuleta maendeleo aliyowaahidi wananchi katika eneo lake la mamlaka, badala ya kuingilia miradi ya mwingine ili kujipatia sifa.
Rais ana wajibu wa kutekeleza ajenda yake ya kitaifa. Magavana nao wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao katika kaunti. Pale ambapo ushirikiano unahitajika, viongozi washirikiane kwa uwazi, kwa kuheshimiana na kwa kuzingatia Katiba bila Malumbano yasio na maana.
Nauliza tu , tulifika lini hapa kama taifa, ambapo miradi ya maendeleo inakuwa uwanja wa vita vya kisiasa badala ya kuwa nyenzo ya kuboresha maisha ya wananchi?
