USALAMA BARABARANI WAIMARIKA SAMBURU, KWALE

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Samburu, katika Kaunti ya Kwale, Patrick Kilonzo Ngoru, amesema usalama barabarani umeimarika kufuatia juhudi za kukabiliana na visa vya uporaji wa mali vinavyohusishwa na ajali za barabarani.
Kilonzo amesema awali, baadhi ya watu walikuwa wakitumia fursa ya ajali za magari, hasa malori yaliyopinduka, kupora mali zilizokuwa zikisafirishwa.
Amesema mafanikio yaliyopatikana yanatokana na ushirikiano kati ya utawala wa eneo hilo, maafisa wa polisi wa trafiki na wananchi katika kuimarisha usalama na kudhibiti vitendo vya uporaji.
Aidha, amesema juhudi za kulinda wasafiri na mali zao zinaendelea, huku akisisitiza umuhimu wa wadau wote kuendeleza ushirikiano huo ili kudumisha usalama barabarani.
Hata hivyo, ameitaka jamii kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu. Pia, amewahimiza wananchi kujiepusha na uporaji wa mali za waathiriwa wa ajali za barabarani.
