Pwani Yetu News Logo

PWANI YETU
NEWS

CRIME

PAUL MACKENZIE KUKABILIWA NA HUKUMU YA ADHABU LEO, SERIKALI YATAKA APEWE ADHABU YA KIFO

Imechapishwa 6 Nov 2026 saa 6:41 AM
3 dakika za kusoma
PAUL MACKENZIE KUKABILIWA NA HUKUMU YA ADHABU LEO, SERIKALI YATAKA APEWE ADHABU YA KIFO

Mhubiri mwenye utata Paul Nthenge Mackenzie na washirika wake wanatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama Kuu ya Mombasa leo, Ijumaa, Novemba 6, 2026, kwa ajili ya kusikiliza maamuzi ya mahakama kuhusu adhabu watakazopatiwa kufuatia kupatikana na hatia ya mauaji ya watu 191, wakiwemo watoto 190, katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Upande wa Mashtaka, unaoongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Ingonga, umeiomba mahakama kumpa Mackenzie adhabu ya kifo, ukitaja uzito wa uhalifu huo, idadi ya waathiriwa na nafasi yake katika kusababisha vifo vya waumini hao.

Katika mawasilisho yake mahakamani, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Jami Yamina, alisema adhabu kali inapaswa kuzingatiwa kutokana na ukubwa wa mauaji hayo na madhara makubwa yaliyozikumba familia za waathiriwa.

Serikali pia imependekeza washirika wengine 27 wahukumiwe kifungo cha maisha gerezani, ikieleza kuwa walikuwa na mchango katika kutekelezwa kwa vitendo vilivyosababisha vifo hivyo.

Hata hivyo, kwa mshtakiwa mwingine, Enos Amanya Ngala, ambaye alikiri kuhusika katika makosa yote 191 ya mauaji, upande wa Mashtaka umependekeza kifungo cha miaka 11 gerezani pamoja na mpango maalumu wa kurekebisha mwenendo wake.

MACKENZIE NA WASHTAKIWA WENZAKE 28 WAPATIKANA NA HATIA

Mnamo Oktoba 19, 2026, Jaji Diana Kavedza wa Mahakama Kuu ya Mombasa aliwapata Mackenzie na washtakiwa wenzake 28 na hatia ya makosa 191 ya mauaji yaliyohusishwa na vifo vya waumini katika msitu wa Shakahola.

Katika uamuzi wake, mahakama ilisema upande wa Mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa wote 29.

Jaji Kavedza alibaini kuwa Mackenzie alikuwa kiongozi wa mfumo wa imani kali uliowashawishi wafuasi wake kufunga kula hadi kufa kwa imani kwamba wangekutana na Yesu.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulionyesha kuwa watoto walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kulazimishwa kufunga, wakifuatiwa na vijana, wanawake na wanaume.

Aidha, baadhi ya waumini waliokataa kufunga au kujaribu kuondoka katika eneo hilo walikabiliwa na vipigo, kuzuiliwa na vitendo vingine vya ukatili.

MKASA WA SHAKAHOLA ULIOITIKISA KENYA

Kashfa ya Shakahola iligonga vichwa vya habari nchini Kenya mwezi Aprili 2023 baada ya polisi kugundua makaburi ya halaiki katika msitu huo ulioko eneo la Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Uchunguzi uliofuatia ulifichua vifo vya mamia ya watu waliokuwa wafuasi wa kanisa la Good News International Ministries lililoongozwa na Mackenzie.

Mackenzie alikuwa akihubiri kuhusu mwisho wa dunia na kuwahimiza wafuasi wake kujitenga na jamii, kukataa elimu ya kawaida na kuepuka huduma za kisasa za afya, akidai kuwa hatua hizo zingewasaidia kufikia ufalme wa mbinguni.

Katika operesheni za uchunguzi, mamlaka zilifukua miili ya zaidi ya watu 400 katika eneo la Shakahola. Hata hivyo, watu 191 ndio waliohusishwa moja kwa moja na mashtaka ya mauaji yaliyosikilizwa katika kesi hii.

Uchunguzi wa kitabibu ulionyesha kuwa baadhi ya waathiriwa walifariki kutokana na njaa, huku wengine wakiwa na dalili za kukosa hewa, kubanwa shingo na majeraha ya kichwa.

MACKENZIE AOMBA MAHAKAMA IWE NA HURUMA

Kabla ya kutolewa kwa hukumu ya adhabu, Mackenzie na washirika wake waliiomba mahakama izingatie mazingira yao binafsi, muda waliokaa rumande na uwezekano wa kubadilika kitabia.

Kupitia mawakili wao, washtakiwa waliomba wapatiwe adhabu isiyozidi miaka 10 gerezani. Walieleza kuwa wamekuwa wakishiriki katika programu za kidini na mafunzo ya kurekebisha mwenendo wao wakiwa kizuizini.

Mackenzie pia aliiomba mahakama kuwaonyesha huruma, akitaja athari ambazo mkasa huo umekuwa nazo kwa familia zilizopoteza watoto na mali.

Hata hivyo, upande wa Mashtaka umesisitiza kuwa adhabu kali inahitajika ili kuzingatia ukubwa wa janga hilo, haki za waathiriwa na umuhimu wa kuzuia matukio kama hayo kujirudia nchini.

Pata habari muhimu moja kwa moja kwenye Email yako

Jiunge na maelfu ya wasomaji wa Pwani Yetu News.

PAUL MACKENZIE KUKABILIWA NA HUKUMU YA ADHABU LEO, SERIKALI YATAKA APEWE ADHABU YA KIFO | Pwani Yetu News