Lunganzi Chai Mangale Atoa Wito wa Umoja kwa Wakazi wa Kwale

Mwaniaji wa kiti cha ugavana wa Kaunti ya Kwale kupitia chama cha ODM, Lunganzi Chai Mangale, amewataka wakazi wa kaunti hiyo kudumisha umoja na ushirikiano, akihimiza kuepuka migawanyiko ya kisiasa kuelekea uchaguzi ujao.
Akizungumza wakati wa kongamano la ODM lililofanyika eneo bunge la Lunga Lunga, Mangale amesema muungano wa upinzani uko imara na umejikita katika kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi wa kijamii au kisiasa.
Mangale amesisitiza umuhimu wa kuweka kipaumbele katika utoaji wa huduma na maendeleo ya jamii, akieleza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kutumiwa kuwagawa wananchi au kudhoofisha ushirikiano miongoni mwa jamii.
Aidha, amewahimiza wakazi wa Kaunti ya Kwale kuunga mkono chama cha Orange Democratic Movement (ODM), akisema chama hicho kinaweza kuchangia katika kuimarisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi katika kaunti hiyo.
Kauli yake inajiri wakati ambapo shughuli za kisiasa zinaendelea kushika kasi huku viongozi na wanasiasa wanaowania nyadhifa mbalimbali wakikutana na wananchi na kujipanga kuelekea uchaguzi ujao.
