TANZANIA: MAHAKAMA KUU KUTOA HUKUMU KATIKA KESI YA UHAINI INAYOMKABILI TUNDU LISSU LEO

Mahakama Kuu ya Tanzania inatarajiwa kutoa hukumu leo, Ijumaa, Novemba 6, 2026, katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu.
Hukumu hiyo inatarajiwa kuhitimisha mchakato wa kesi iliyodumu kwa takribani mwaka mmoja na kuvutia mjadala mkubwa wa kisiasa, kisheria na kijamii ndani na nje ya Tanzania.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Lissu alitoa matamshi Aprili 3, 2025, katika makao makuu ya CHADEMA jijini Dar es Salaam, ambayo yanadaiwa kuwa na nia ya kuwashawishi wananchi kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mashtaka yanadai kuwa matamshi hayo yalilenga kuchochea uasi na kuvuruga mchakato wa uchaguzi ili kushinikiza mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Hata hivyo, Lissu ameyapinga madai hayo, akisisitiza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka la uhaini dhidi yake kwa mujibu wa sheria.
Katika utetezi wake, Lissu alipinga uaminifu na uhalali wa baadhi ya ushahidi uliowasilishwa na mashahidi wa mashtaka. Alieleza kuwa matamshi yake yalikuwa sehemu ya harakati za kisiasa za kutetea mageuzi, kupatikana kwa Katiba mpya, uchaguzi huru na wa haki pamoja na kuimarisha utawala wa sheria nchini Tanzania.
Katika mwenendo wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha jumla ya mashahidi 17, huku upande wa utetezi ukiwasilisha mashahidi watano. Pande zote mbili zilihitimisha hoja zao za mwisho Septemba 29, 2026.
ADHABU ANAYOWEZA KUKABILIWA NAYO TUNDU LISSU AKIPATIKANA NA HATIA

Miongoni mwa masuala yanayofuatiliwa kwa karibu katika kesi hiyo ni adhabu ambayo Lissu anaweza kupewa iwapo mahakama itamtia hatiani.
Kifungu cha sheria kinachotumika katika shtaka hilo kinataja adhabu ya kifo kwa kosa la uhaini.
Hata hivyo, upande wa mashtaka umeeleza kuwa mahakama ina mamlaka ya kuamua adhabu inayofaa kwa kuzingatia mazingira ya kesi, na kwamba hukumu ya hatia haimaanishi moja kwa moja kuwa adhabu ya kifo itatolewa.
Kwa upande wake, Lissu amekuwa akisisitiza kuwa kifungu hicho kinaweka wazi adhabu ya kifo kwa kosa hilo.
Uamuzi wa mahakama unatarajiwa kuwa na athari kubwa katika mazingira ya kisiasa na kisheria nchini Tanzania, huku kesi hiyo ikiwa miongoni mwa mashauri yanayofuatiliwa kwa karibu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Hukumu hiyo pia inatarajiwa kuvuta hisia za wadau wa demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria, ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi hiyo.
